Baada ya uvamizi wa Waarabu Ujaemi wkatawaliwa kwa muda kama sehemu ya ukhalifa wa Uislamu lakini baada ya karne kadhaa nasaba za kieneo zilichukua utawala kwa jina la khalifa ila hali halisi kama watawala wa kujitegemea.
Baada ya uvamizi wa Wamongolia nasaba ya wana wa Timur iliunganisha Uajemi pamoja na Afghanistan na Asia ya Kati.
Tangu mwaka 1600kitovu cha utawala kilirudi Uajemi wenyewe chini ya nasaba za Safawi na Khadjari.
Uhusiano na nchi za magharibi, na hasa Marekani, umekuwa mgumu tangu mapinduzi, hasa baada ya wanafunzi Waajemi kushambulia ubalozi wa Marekani mjini Teheran na kuwateka Wamarekani kama makole. Fatwa ya Ayatollah Khomeini kudai kifo cha mwandishiSalman Rushdie iliongeza sifa za ukali za Uajemi.
Uajemi ni Jamhuri ya Kiislamu inayoongozwa na katiba yenye sehemu za kidemokrasia na sehemu za kidini.
Mamlaka kuu iko mikononi mwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi anayesimamia siasa ya nchi kwa jumla; yeye ni amiri jeshi mkuu na msimamizi mkuu wa huduma ya usalama; pia anaratibu siasa ya nje. Anateua wakuu wa jeshi, redio na televisheni, viongozi wa salat wa msikiti mkuu katika kila mji, jaji mkuu na mwendesha mashataka mkuu halafu nusu ya wajumbe wa Halmashauri ya Walinzi wa Katiba wanaokubali au kukataa sharia zote zilizopitishwa bungeni wakiwa na mamlaka kusimamisha wagombea kwa uchaguzi wa kitaifa. Anaweza kumwachisha rais. Kiongozi mkuu huchaguliwa na Mkutano wa Wataalamu wa Uongozi kwa muda wa maisha yake. Ayatollah Khamenei ni Kiongozi Mkuu wa pili tangu mapinduzi ya Kiislamu.
Serikali inayoongozwa na rais wa Uajemi aliye na nafasi ya pili baada ya Kiongozi Mkuu. Huchaguliwa na wananchi wote kwa kipindi cha miaka 4 na anaweza kuchaguliwa upya. Wagombea wanahitaji kukubaliwa na Halmashauri ya Walinzi wa Katiba. Rais anaongoza serikali na kazi yake. Katika mambo ya siasa ya nje, jeshi na siasa ya nyuklia yuko chini ya mamlaka ya kiongozi mkuu.
Bunge inayoitwa "majlis" ina wabunge 290 waliochaguliwa kwa muda wa miaka 4. Wagombea wote wanahitaji kibali cha Halmashauri ya Walinzi wa Katiba. Majlis inatunga sheria za nchi na kukubali makisio ya serikali na mikataba ya kimataifa. Sheria zote zilizopita bungeni zinahitaji tena kibali cha halmashauri ya walinzi.
Halmashauri ya Walinzi wa Katiba ni chombo muhimu sana kinachohakikisha mamlaka kuu ya kiongozi mkuu. Ina wajumbe 12 ambao ni wanasheria. 6 wanateuliwa moja kwa moja na Kiongozi Mkuu. 6 wengine wanachaguliwa na bunge kati ya majina wanaopelekwa mbele na jaji mkuu - anayeteuliwa na Kiongozi Mkuu. Kwa hiyo kiongozi mkuu anaamua juu ya wajumbe wote waliomo katika halmashauri hii, hakuna anayeweza kuwa mjumbe bila kibali chake ama moja kwa moja au kupitia jaji mkuu aliyeteuliwa naye.
Uajemi umegawiwa kwa mikoa 31 inayoitwa "ostan" chini ya gavana anayeteuliwa na rais. Kila mkoa huwa na wilaya (shahrestan) na ngazi ya chini zaidi ni mitaa (bakhsh). Chini ya mitaa kuna kata (dehestan) zinazojumlisha vijiji kadhaa.
Leo hii takriban asilimia 90 za wakazi ni Waislamu Washia. Karibu 10% ni Wasunni, hasa katika maeneo karibu na mipaka; kiutamaduni Wasunni wengi ni Wakurdi, Wabaluchi au Waturkomani.
Wafuasi wa dini nyingine kwa jumla ni kama 1% ya wakazi wote. Kundi kubwa ni Bahai lakini dini yao ilipigwa marufuku baada ya mapinduzi ya Kiislamu. Kundi linalofuata ni Wakristoː kati hao kundi kubwa ni Waarmenia, halafu Wakaldayo. Wayahudi wa Uajemi ni kundi kubwa kati ya nchi zote za Kiislamu wa mashariki ya kati (0.01%). Wazoroasta wamebaki pia (0.03%). Kundi dogo sana ni Wamandayo wanaoitwa pia wafuasi wa Yohane Mbatizaji.
1. Nchi ina maeneo katika Asia na Ulaya. 2. Nchi iko Asia lakini inahesabiwa pia kati ya nchi za Ulaya kwa sababu za historia au utamaduni. 3. Eneo la pekee la China.
Makala hii kuhusu maeneo ya Asia bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Uajemi kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.