Kamuzu Banda alizaliwa karibu na Kasungu, Malawi iliyokuwa wakati ule sehemu ya eneo lindwa la Afrika ya Kati ya Kiingereza (baadaye Nyasaland). Wazazi walikuwa Mphonongo Banda na Akupingamnyama Phiri. Tarehe ya kuzaliwa haijulikani ilhali wakati ule hakukuwa na utaratibu wa kuandikisha watu. Alikubali baadaye matokeo ya utafiti wa rafiki kutoka Marekani aliyekadiria ya kwamba alizaliwa mnamo Machi au Aprili 1898.[1][8]
Jina lake Kamuzu lamaanisha "mzizi mdogo" kwa sababu alizaliwa baada ya mama yake kutumia dawa ya mitishamba kwa kusudi la kupata mimba[2]. Banda lilikuwa jina la baba yake, na jina la Hastings alijiongezea baada ya kubatizwa kwa heshima ya mmisionari mmoja kutoka Uskoti aliyependwa naye.
Alisoma kwa miaka 3 kwenye Wilberforce Institute iliyokuwa chuo cha Kanisa la A.M.E. akaendelea kwa miaka 2 Bloomington, Indiana, kwa maandalizi ya masomo ya tiba.
Alizunguka nchini akiwahutubia watu na kudai uhuru wa Unyasa[3]. Kutokana na muda mrefu wa kukaa mbali na nyumbani alihitaji wafasiri maana alishindwa mwanzoni kutumia Lugha mama yake.
Wananchi wengi walimfuata na hadi mwaka 1959 harakati ya uhuru iliongezeka kiasi kwamba serikali ilitangaza hali ya dharura. Banda alikamatwa na kuwekwa jela kwa miezi 11. Chama cha NAC kilipigwa marufuku lakini wanachama nje ya gereza waliunda badala yake chama cha "Malawi Congress Party" (MCP) na kumtangaza Banda kuwa mwenyekiti ingawa bado alikaa jela.
Wakati huo wanasiasa katika Uingereza walianza kukazia uhuru kwa makoloni yake. Kwa hiyo Banda aliachishwa gerezani kwenye Aprili 1960 akapelekwa London kwa majadiliano kuhusu uhuru wa nchi.
Baada ya uchaguzi wa Agosti 1961 ulioleta kura nyingi kwa chama chake Banda alikuwa waziri wa ardhi na serikali za mitaa. Tarehe 1 Februari 1963 alikuwa waziri mkuu wa Nyasaland.
Mwaka 1964 aliongoza nchi kwenye uhuru kamili. Banda aliamua kubadilisha jina kutoka Nyasaland kuwa "Malawi".
Kuelekea udikteta
Wakati wa Agosti na Septemba 1964 Banda alijikuta mara ya kwanza mbele ya upinzani wa mawaziri wengi. Walilalamika juu ya Banda kutoshauriana nao akifanya maazimio, kuendelea kwa uhusiano wa kidiplomasia na Afrika Kusini (iliyofuata siasa ya apartheid) na Ureno iliyotawala makoloni ya Msumbiji n.k.
Banda aliachisha mawaziri watatu tarehe 7 Septemba. Mawaziri wengine waliwafuata wakijiuzulu. [4]Maandamano nchini yalifuata na wafuasi wa Banda walipigana na hao wa mawaziri. Mawaziri wengi waliondoka nchini. Wawili walijaribu kuingia pamoja na wanamgambo wenye silaha kutoka Msumbiji lakini walishindwa.
Mwaka 1970 alitangazwa kuwa mwenyekiti kwa maisha yote wa chama cha MCP. Hatua hii ilifuatwa na Banda kuwa rais wa taifa kwa maisha yake yote. Umoja wa vijana wa chama cha MCP ulihakikisha kukomeshwa kwa kila upinzani nchini pamoja na vyombo vya dola.
Wote walipaswa kumtaja kwa jina la "His Excellency the Life President Ngwazi Dr. H. Kamuzu Banda" kwa kuongeza "Ngwazi" ambalo ni neno la Chichewa lenye maana ya "shujaa". Kutamka maneno ya ukosoaji dhidi ya rais ilikuwa hatari.
Banda alifaulu kutunza amani nchini wakati wa utawala wake lakini aliongoza kama dikteta. Mwaka 1983 mawaziri watatu wa serikali yake waliuawa. Banda mwenyewe alianzisha majadiliano kuhusu kukubali vyama vingi nchini. Mawaziri watatu waliunga mkono hoja hii na mara moja rais aliachisha baraza lote la mawaziri akaita mkutano wa bunge na kuachisha wabunge wote. Mawaziri watatu walifungwa katika chumba bungeni na kupigwa. Mbunge mmoja aliingia katika chumba hiki na kuwaona wakiteswa alikamatwa pamoja nao. Wote wanne walipatikana wamekufa katika gari la Peugeot lililopinduka. Serikali ilizuia kufunguliwa kwa majeneza wakati na mazishi yaliyotokea usiku. Walitangazwa kuwa wahanga wa ajali lakini baadaye ilijulikana waliuawa kwa kupiga misumari katika vichwa vyao kabla ya kuweka maiti katika gari na kulisukuma katika korongo.[5]
Anguko
Hadi mnamo 1990nchi za magharibi zilisaidia au angalau kuvumilia serikali ya Banda kwa sababu alikuwa mpinzani wa ukomunisti, pia kati ya nchi chache za Afrika zilizoendelea kuwa na uhusiano na Afrika Kusini. Lakini kuporomoka kwa ukomunisti kulisababisha badiliko. Wafadhili wa miradi ya maendeleo walidai mabadiliko ya kuheshimu haki za binadamu. Serikali ya Uingereza ilisimamisha usaidizi wote kwa Malawi.
Katika Machi 1992 maaskofu Wakatoliki wa Malawi walitunga waraka kwa Wakristo walipotamka ukosoaji wa Banda na serikali. Wanafunzi wa vyuo walichukua upande wa maaskofu na kuandamana. Vyuo vikafungwa.
Hadi Oktoba 1992 Banda alipaswa kukubali kura ya wananchi kuhusu swali la kukubali vyama vingi. Kura hii ilileta asilimia 64 kwa ajili ya demokrasia ya vyama vingi. Mwaka huohuo halmashauri mpya ilitangaza katiba mpya na kuondoa "urais wa maisha". Jeshi la Malawi lilivamia vituo vya Umoja wa Vijana wa MCP na kukamata silaha zote zilizowahi kupewa kama mkono wa utawala wa chama [6]. Katika uchaguzi wa mwaka 1994 Banda aligombea tena urais lakini alishindwa na Bakili Muluzi. Chama kipya cha Muluzi kilipata wabunge wengi.
Mwaka 1995 Banda alikamatwa na kupelekwa mahakamani kwa mashtaka ya kuhusika katika mauaji ya mawaziri ya mwaka 1983[7]. Aliachishwa kutokana na upungufu wa ushahidi.
Banda aliendelea kuwaangalia Wamalawi kama "watoto wa siasa" akatabiri ya kwamba wanahitaji "mkono wa chuma".
Mwaka 1997 alingonjeka akapelekwa kwa matibabu Afrika Kusini alipofariki tarehe 25 Novemba 1997 akiwa na umri wa miaka 99 hivi.
Tanbihi
↑Dr Banda - Biography, uk. 4, iliangaliwa kwenye tovuti ya scribd.com mnamo Januari 2017
"Banda, Hastings Kamuzu". Oxford Dictionary of National Biography (2004 ed.).
Hulec, Otakar and Jaroslav Olša, jr (2008). Dějiny Zimbabwe, Zambie a Malawi (in Czech, translation of title: History of Zimbabwe, Zambia and Malawi), Nakladatelství Lidové noviny.
Lwanda, John Lloyd, (1993). Kamuzu Banda of Malawi: A Study in Promise, Power, and Paralysis, Dudu Nsomba Publications.
Meredith, Martin (2005). The Fate of Africa: From the Hopes of Freedom to the Heart of Despair, Public Affairs.
Muluzi, Bakili (with Yusuf M. Juwayeyi, Mercy Makhambera, Desmond D. Phiri), (1999). Democracy with a Price: The History of Malawi since 1900. Jhango Heinemann, Blantyre.
Mwakikagile, Godfrey, (2006). Africa After Independence: Realities of Nationhood. Johannesburg, South Africa: Continental Press.
Ross, Andrew C. (2009). Colonialism to cabinet crisis: a political history of Malawi, African Books Collective, 2009 ISBN 99908-87-75-6. This gives extensive biographical detail on Hastings Banda.
Rotberg, Robert I, (1965). The Rise of Nationalism in Central Africa. Cambridge: Harvard University Press.
Shaw, Karl (2005) [2004]. Power Mad! (kwa Czech). Praha: Metafora. ISBN80-7359-002-6. {{cite book}}: Unknown parameter |trans_title= ignored (|trans-title= suggested) (help)CS1 maint: unrecognized language (link)
Short, Philip (1974). Banda. London: Routledge & Kegan Paul.
van Donge, Jan Kees (1995). Kamuzu's legacy: the democratisation of Malawi. African Affairs, Vol 94, No 375.