Wagogo wamekuwa wakijenga nyumba ambazo kwa Kigogo huitwa "itembe". Tangu zamani kuta za tembe zilijengwa kwa fito (kwa Kigogo hutamkwa sito) zilizosukwa kwa kupisha kuzuia mwanga na maji. Vipande vya kuta vilivyosukwa kwa sito vinaitwa "izizi".
Tembe huezekwa kwa udongo ambao hushikiliwa na miti midogomidogo iitwayo "walo". Walo huwa inashikiliwa na miti mikubwa kidogo iitwayo "mahapa" na mahapa hushikiliwa na miti mikubwa iitwayo "michichi". Michichi ambayo ndiyo hubeba uzito wote hushikiliwa na nguzo kubwa za miti imara na migumu. Nguzo hizo hutiwa "masumbilili".
Kwa miaka ya karibuni kuta za tembe hujengwa pia kwa matofali yanayotengenezwa kwa udongo
Shughuli za uchumi
Wagogo ni miongoni mwa makabila ya wakulima na wafugaji kwa asili na hufuga mifugo kama ng'ombe, mbuzi na kondoo. Kwa Kigogo wanyama hao huitwa "ng'ombe, mhene na ngholo" pamoja na punda "ndogowe" kwa ajili ya ubebaji mizigo na wakati mwingine kulimia wakitumika kukokota majembe ya kukokotwa, kama watumikavyo ng'ombe pia.
Sambamba na shughuli hiyo, kilimo ndiyo shughuli kubwa na ya wengi, ijapokuwa kwa miaka mingi imekuwa ikiathiriwa na kiwango kidogo cha mvua zinazonyesha kutokana na jiografia ya mikoa hiyo miwili, yaani Dodoma na Singida.
Mazao yanayolimwa kwa wingi ni mahindi, mtama, uwele, na lugugu. Siku za hivi karibuni umeingia mtama unaokomaa kwa muda mfupi kama vile serena, lulu, tegemeo, masia, okoa, n.k., muhogo kiasi na katika maeneo machache mpunga na mzabibu, zao ambalo ni mahususi kwa biashara.
Chakula kikuu
Wagogo hula ugali wa uwele kama chakula kikuu na huchukulia ugali wa mahindi na mtama kama chakula laini na chepesi kisicho na nguvu.
Miaka ya zamani mlo wa kawaida wa Mgogo mwenye uwezo (yaani mwenye ng'ombe) ulihusisha ugali, maziwa, mafuta ya ng'ombe, kwa kigogo samuli na mboga kama mlenda ("ilende"), safwe, cidingulilu, nyakifwega, muhilile, sanghala, munzimwa, cipali, ihaji, sagulasagula, ikuwi, fwene, nghalabwajila (hasa wakati masika inapoanza) n.k.
Kwa sasa Wagogo wamekuwa wakila chakula cha kawaida kama makabila mengine nchini Tanzania.
Lafudhi ya lugha
Kabila la Wagogo lina lahaja ndani yake ambazo hutofautiana kutoka moja hadi nyingine kwa jinsi ambavyo hutamka maneno, yaani huongeza na kupunguza baadhi ya matamshi kwenye neno, na pia katika msamiati. Kwa ujumla kuna lahaja zipatazo 4, ambapo lahaja za Cinyambwa na Cinyaugogo ndizo hujulikana zaidi.
2. Wanyaugogo - hawa huongea lafudhi iitwayo Chinyaugogo. Wanyaugogo ambao ndio wanaowakilisha kundi kubwa sana hutokea vijiji vya mashariki na kusini kwa mji wa Dodoma na pia wilaya ya Mpwapwa. Kwa sababu mtemi Mazengo alikuwa Mnyaugogo kutoka Mvumi, mahali ambapo palijengwa kijiji kinachoitwa Mvumi Makulu (kwa maana kwamba ndipo ilipokuwepo Ikulu ya Mtemi), inaaminika kuwa lafudhi hii ndicho Kigogo cha asili isiyoathiriwa na lugha za nje.
Mifano - matamshi: - vipi? = nhaule?
-msamiati - panda darini = unanuce kitembe
3. Wetumba - Hawa ni Wagogo walioathiriwa Kigogo chao na Kikaguru. Hupatikana katika wilaya za Kongwa na Mpwapwa
Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Wagogo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.